Serikali ya Kaunti ya Mombasa imesema kuwa imewakamata maafisa wawili wa kaunti wanaodaiwa kujihusisha na visa vya ufisadi.
Maafisa hao wa kaunti wanadaiwa kuhusika na visa vya kuchukua hongo madai yaliyoibuliwa na Peter Oluoch, kutoka katika kampuni ya Vipingo Ridge.
Katika taarifa kwa vyombo vya habari siku ya Jumanne, Gavana wa Kaunti ya Mombasa Hassan Joho alisema waliamua kuchukua hatua ya haraka ili kuwanasa maafisa hao wanaochafulia serikali jina.
“Maafisa wetu wa kufanya uchunguzi walichukua hatua hiyo ili kubaini ukweli wa madai hayo yaliyowasilishwa kwetu,” alisema Joho.
Maafisa hao wa kaunti waliwekwa kwenye mstari na kisha mlalamishi akapewa fursa ya kukagua mmoja baada ya mwingine ili kuwatambua wale waliotekeleza kosa hilo.
Hatimaye, walifanikiwa kuwatambua wawili ambao baadae watafikishwa mahakamani hivi karibuni ambapo watashkiwa kwa makosa ya ufisadi.
Wakati huo huo, Gavana Joho alisema kuwa serikali yake itasimama wima kuhakikisha kuwa yeyote atakayepatikana akitekeleza ufisadi anakabiliwa na sheria kali.
“Serikali yangu haitakubali ufisadi wa aina yoyote na afisa wa kaunti atakayepatikana na makosa lazima apatane na mkono wa sheria,” aliongeza Joho.
Aidha, gavana huyo aliwasihi wananchi kuripoti visa vya ufisadi moja kwa moja hadi katika ofisi yake.