Wakaazi wa Nyamakoroto wadi ya Gesima eneo bunge la Kitutu Masaba, kaunti ya Nyamira, wamewaomba maafisa wa polisi kutochukua hongo kutoka kwa wagema.
Wakaazi hao walisema wagema wanaposhikwa wanastahili kulipa faini ya kiwango cha juu kama njia moja ya kukomesha pombe haramu katika lokesheni hiyo.
Wakiongea siku ya Jumatatu katika kituo cha kupimia chai cha Nyamakoroto, wakulima wa majani chai walisema kuwa viwango vya kilimo katika eneo hilo vimerundi chini kutokana na pombe haramu katika lokesheni hiyo ya Nyamakaoro na ile ya Mochenwa.
kwa sasa wameomba askari wa utawala kutochukua hongo kutoka kwa wagema na kuwaruhusu kuendelea kutengeneza pombe haramu.
“Maafisa wa polisi wanapochukuwa hongo kutoka kwa wagema, wagema hoa huwa na nafasi ya kuendelea kutengeneza pombe hiyo kwani wanaelewa kuwa hata wakitengeneza watalipa kitu kidogo ili kuendeleza biashara hizo, ”alisema Daniel Nyakanga, mkaazi wa Kijiji cha Nyamakoroto.
Aidha, walisema kuwa wanoshikwa na pombe hiyo wanastahili kutozwa faini ya juu ili iwe funzo kuwa wakiendelea kutengeneza pombe hiyo watakuwa wanatozwa faini ya kiwango cha juu.
“Naomba kuwa wagema wakishikwa wawe wakitozwa faini ya kiwango cha juu kama njia moja ya funzo kuwa wakiendelea kupika watakuwa wanatozwa zaidi ya zile pesa wanazopata," alisema, Ezina Moraa mkaazi.
Naibu chifu Robert Monda alisema kuwa wanaendelea kupiga vita pombe hiyo ili kuhakikisha kuwa imeeisha.
Haya yanajiri siku moja tu baada ya mwanaume mmoja kupatikana katika sehemu ya Kegati Kaunti ya Kisii akiwa amekufa kutokana na kubugia pombe haramu.