Share news tips with us here at Hivisasa

Baadhi ya maafisa wa polisi kutoka Pwani wameshtumiwa kwa kujihusisha na walanguzi na watumizi wa dawa za kulevya na kuchangia kuenea kwa biashara hiyo haramu.

Kulingana na Mwenyekiti wa Chama cha Maendeleo ya Wanawake katika Kaunti ya Mombasa Afiya Rama, baadhi ya maafisa wa polisi wanaopewa habari kuhusu washukiwa wa ulanguzi wa mihadarati huwasiliana na jamaa hao na kuwajulisha habari hizo kisha jamaa hao hutoweka.

Akiongea na mwandishi huyu mjini Mombasa siku ya Jumatatu, Rama alisema kwamba ni lazima kwa maafisa wa polisi kujitolea kimasomaso katika kupiga vita utumizi wa mihadarati ili kuwanasua vijana wengi waliyojitosa katika janga hilo, licha ya wakazi kujitokeza kuunga mkono kampeni ya kuangamiza mihadarati.

Aidha, alisema kwamba hatua hiyo imechangia pakubwa katika kuleta hofu kwa wakazi katika Kaunti ya Mombasa kwa jumla hali ambayo inafaa kuchunguzwa na maafisa husika kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

“Tunasikitishwa na jinsi baadhi ya maafisa wa polisi wanavyoshirikiana na walanguzi wa dawa za kulevya kwa kuwafahamisha habari watoweke, ilhali sisi tuko katika mstari wa mbele wa kukabiliana na mihadarati. Hatua hiyo imetia wakazi wengi hofu ya maisha yao kwamba huenda wakavamiwa kwa kutoa habari hizo,” alisema Rama.

Mwenyekiti huyo wa chama cha maendeleo ya wanawake amependekeza hatua kali zichukuliwe kwa walanguzi wa mihadarati katika eneo la Pwani ili kusitisha kukithiri kwa biashara hiyo haramu pamoja na kuwaokoa vijana wadogo.