Baadhi ya maafisa wa trafiki waliofika mbele ya jopo la ukaguzi wamekabiliwa na wakati mgumu kueleza jinsi walivyojipatia mali wanazomiliki.
Afisa Cyrus Wanyonyi, aliyefika mbele ya jopo hilo siku ya Jumanne, alikabiliwa na wakati mgumu kueleza umiliki wake wa shilingi milioni 82.
Wanyonyi alisema fedha hizo zinatokana na umiliki wake wa shamba la sukari pamoja na ufugaji miongoni mwa biashara nyengine.
Hata hivyo, jopo hilo lilishangazwa na jinsi afisa huyo wa trafiki alivyojipatia hekari za shamba hilo, pamoja na uhamisho wake wa fedha mara kwa mara kutumia huduma ya simu ya Mpesa.
Inspekta Lucy Wanjiru, kutoka kituo cha polisi cha Likoni, kwa upande wake alitakikana kueleza jinsi alivyojipatia umiliki wa matatu saba za abiria, pamoja na kumiliki akaunti sita tofauti katika banki mbali mbali.
Inspekta huyo alielezea jopo hilo kuwa alinunua matatu hizo kwa kutumia pesa za mkopo pamoja na fidia aliyolipwa baada ya baadhi ya gari zake kuhusika katika ajali.
Jumla ya maafisa 238 wa trafiki kutoka kanda ya Pwani watafanyiwa ukaguzi huo.
Jopo hilo linaongozwa na Tume ya kitaifa ya huduma kwa polisi NPSC chini ya uongozi wa Johnston Kavuludi.