Machifu na mamaibu wao katika taarafa ya Nyamusi wilaya ya Nyamira kazkazini wanahofia maisha yao, wakisema huwa wanawatia mbaroni majambazi na washukiwa wa uhalifu na baadaye wanaachiliwa huru na mahakama kwa kulipa faini ama kuwekewa bondi.
"Tunapowafikisha washukiwa ana majambazi wakiwa na ushahidi kwa polisi ama mahakamami, wao huachiliwa kwa kulipa bondi na kurudi kijijini na kutisha ya kwamba tutakiona cha mtema kuni," alisema chifu mmoja ambaye hakutaka jina lake litajwe.
"Majambazi waliwauwa mbwa wangu wanne na kuhadharisha maisha yangu, ikanilazimu nihame nyumbani na kuishi karibu na Jabera ili kuwa salama," alisema naibu wa chifu mmoja.
Machifu hao na manaibu wao sasa wanaiomba serikali kubuni sheria ambayo itawafanya majambazi na washukiwa walio na ushahidi kufungiwa ndani ili kujifunza maadili mema wakiwa gerezani.
"Tunaiomba serikali kubuni kifungu ambacho kitawatia majambazi hawa ndani bila kulipa faini ama kutoa bondi ili wajifunze maadili mema kule gerezani kuliko kututishia maisha," alisema chifu mwingine.
Maafisa hao walikuwa wakizungumza na mwandishi huyu katika kata ya Bokeira siku ya Jumatatu.