Share news tips with us here at Hivisasa

Usalama ni jukumu la kila mtu. 

Hapo jana machifu, manaibu pamoja na maafisa wa usalama kutoka kaunti ya Kisii walikutana katika hoteli ya Ufanisi mjini Kisii kwa mafundisho jinsi wanafaa kutumia mpango wa Nyumba Kumi kuimarisha usalama.

Mkutano huo ulipangwa na kitengo cha Jopo la Kitaifa la Polisi wa Mitaa (National Task force for Community Policing) kutoka Nairobi uliwakutanisha machifu zaidi ya mia mbili na manaibu wao.

Akizungumza katika mkutano huo naibu kaunti kamishina wa Kisii bwana Peter Mbugi amesema ni hatua ambayo itasaidia pakubwa kuimarisha usalama mashinani.

“Mpango huu ulianzishwa kitambo, kaunti zingine zimefundishwa na leo ilikuwa zamu yetu. Lengo la mkutano huu ni kuwafundisha maafisa wote wa usalama wakiwemo polisi na machifu ili washiririkiane kwa pamoja kuimarisha usalama," alisema Mbugi.

"Usalama unaanza na mtu binafsi. Nyumba kumi ni mpango ambao utasaidia watu kujuana pale kijijini hata hapa mjini kwa ploti mbalimbali. Jirani ajue mwenzake anachofanya. Tukifanya hivyo tutakuwa tumemaliza mambo ya ukosefu wa usalama," alidokeza Mbugi.

“Kwa hivyo machifu wote ambao wamefika hapa leo wamefundishwa na tunawaomba wayatilie maanani mafundisho haya ili mkenya aliye pale chini ajisikie kuwa huru bila wasiwasi," aliongeza Mbugi.

"Pia tunataka wachague vijana wale wanaweza kufundishwa waje tuwafundishe ili nao waende kufundisha wengine pale vijijini,"  aliongeza Mbugi.

Maafisa hao pia wamefurahia kupokea mafunzo hayo huku wakisema watayatilia maanani kwa usalama wa mwananchi.