Maafisa wawili wa usalama wanazuiliwa katika kituo kimoja cha polisi mjini Mombasa baada ya kutiwa nguvuni na maafisa wa Tume ya Maadili na Kupambana na Ufisadi nchini EACC kwa tuhuma za ufisadi.
Inadaiwa kuwa Daniel Chacha, ambaye ni askari wa Kaunti ya Mombasa alitiwa nguvuni katika eneo la Soko la Kongowea baada ya kupatikana akiitisha rushwa ya shilingi elfu tano, huku afisa wa idara ya upelelezi katika Kaunti ya Taita Taveta akitiwa nguvuni kwa madai ya kupokea shilingi elfu 25, ili kutatua kesi inayomkabilia mwakilishi wadi na afisa tawala.
Akizungumza siku ya Jumanne, afisa wa Tume ya EACC anayesimamia eneo la kusini mwa Pwani na Mombasa Simon Cherpka, alisema kuwa kupitia juhudi za maafisa wa tume hiyo kwa ushirikiano na wananchi, wamefanikiwa kuwatia nguvuni maafisa hao huku akiwashinikiza wananchi kujitolea kusitisha ufisadi.
"Tunawashukuru maafisa wetu na wananchi kwa kutuwezesha kuwatia nguvuni maafisa hawa. Hatua hiyo inaonyesha wazi kuwa wananchi wamechoka na maafisa wafisadi,” alisema Cherpka.
Kwa upande wake, afisa mkuu wa askari katika Kaunti ya Mombasa Karisa Changawa alisema kuwa kaunti hiyo itahakikisha kuwa ufisadi unasitishwa na atakayepatikana atachukulia hatua za kisheria.
Wawili hao watafikishwa mahakamani siku ya Jumatano kufuatia agizo kutoka kwa Mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma nchini Keriako Tobiko.