Huku ikibakia miezi miwili maonyesho ya kilimo na biashara kuandaliwa katika eneo la Nyanza Kusini, mwandalizi mkuu wa maonyesho hayo Julius Bosire ameyaomba mashirika kujitokeza ili kujiandikisha mapema.
Bosire alikuwa akizungumza na waandishi wa habari katika uwanja wa michezo wa Gusii walipokuwa wakipangilia mikakati ya maonyesho hayo, na aliwataka wawekezaji wa benki, mashirika ya vyama vya fedha na wakulima kujitokeza na kutuma maombi yao mapema ili kupata nafasi mwafaka ya kutangaza bidhaa zao.
“Mashirika yote na vilevile wakulima husika tunawaalika katika maonyesho haya katika uga huu wa Gusii, hatubagui" alisema Bosire huku akisisitiza umuhimu wa kujisajili mapema kuwa inawezesha kupangilia nafasi iliyoko virahisi.
Maonyesho hayo alisema yameweza kuvutia wawekezaji wakuu wa kifedha kama vile Benki Kuu ya Kenya.
Maonyesha haya hufanywa kila mwaka na hushirikisha maeneo yote ya Gusii, Migori, Homabay na mashirika mengine ambayo hualikwa na waandalizi.
Bosire pia alionyesha kuridhika kwake, kwani kutakuwa na wawekezaji wengi msimu huu ikizingatiwa kuwa wameanza miezi miwili mapema kinyume na ilivyokuwa miaka mingine ya awali, ambapo walikuwa wanaanza siku chache kabla ya maonyesho hayo.
“Nina matumaini makubwa sana msimu huu kuwa tutakuwa na mafanikio zaidi kinyume na ilivyokuwa zamani tulipokuwa tukianza tukiwa tumechelewa,” alisema Bosire huku akitabasamu.