Bodi ya utalii nchini imesema kuwa maandamano dhidi ya Tume ya IEBC yanaathiri sekta ya utalii.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Haya yanajiri baada ya Kaunti ya Mombasa chini ya uongozi wa Gavana Hassan Joho kushiriki maandamano hayo ya kushinikiza kubanduliwa kwa Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC, siku ya Jumatatu kwa mara ya kwanza.

Akiwahutubia wanahabari siku ya Jumatatu, kaimu mkurugenzi wa Bodi ya Utalii Bi Jacinta Nzioka alisema kuwa maandamano hayo yatakandamiza ukuaji wa sekta hiyo, na kuregesha nyuma hatua walizokuwa wamezipiga.

"Asilimia 20 ya matarajio ya watalii wa nchi za kigeni mwaka huu hayataweza kuafikiwa na itabakia ndoto tu ikiwa maandamano haya yataendelea,” alisema Bi Nzioka.

Wakuu wa bodi hiyo wameitisha mkutano wa dharura na washika dau kujadili maandamano hayo waliyosema yanaadhiri utalii ambao ulikuwa umeanza kunawiri baada ya pigo la maswala ya usalama nchini,” alisema Bi Nzioka.

"Tutakuwa tunayaangazia maswala ya matangazo ili kuweza kupiga jeki sekta ya utalii. Kuhusu swala la Tume ya IEBC, kuna katiba ambayo ina sheria mwafaka ya kufuata na kusuluhisha utata huu bila maandamano,” alisema Nzioka.