Kinara wa Cord Raila Odinga amewataka viongozi wenza kuendeleza maandamano dhidi ya Tume ya IEBC baada ya makataa waliyopeana kwa serikali kuu kuisha.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza siku ya Jumamosi kwenye hafla ya kupeana hundi za basari kwa zaidi ya shule elfu nane katika uwanja wa maonyesho wa Mkomani mjini Mombasa, Raila alizungumzia kwa uzito haja ya kubanduliwa kwa maafisa wa Tume huru ya uchaguzi na mipaka IEBC.

“Licha ya serikali kutangaza kukamtwa kwa yeyote atakayepatikana akiandamana, bado haki za kuandamana zinalindwa kikatiba kama njia moja wapo ya mwananchi kuwasilisha malalamishi,” alisema Raila.

Raila alisisitiza kuwa maandamano hayo yataendelea kama ilivyoratibiwa kwa kuwa hiyo ndiyo haki ya nchi yenye demokrasia.

Aidha, kiongozi huyo wa Chama cha ODM alimpongeza Gavana wa Mombasa Hassan Joho kwa utendakazi wake katika juhudi za kuimarisha viwango vya elimu katika kaunti ya Momabasa.

Hafla hiyo ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali kutoka mrengo wa Cord.