Serikali ya Kaunti ya Kisii imeweka mikakati kabambe ya kuhakikisha kuwa wanaoishi na ulemavu wanasaidiwa ili waweze kujiendeleza kimaisha.
Akiongea siku ya Jumatano katika hafla ya kuwafadhili mazerezeru miwani katika ukumbi wa utamaduni na michezo mjini Kisii, Naibu Gavana wa Kaunti ya Kisii Joash Maangi alisema kuwa serikali ya kaunti imeweka mikakati kabambe ya kusaidia wanaoishi na ulemavu katika Kaunti ya Kisii kama njia moja ya kuinua viwango vyao vya maisha.
“Serikali ya kaunti ya Kisii imeweka mikakati kabambe ya kuwasaidi wanaoishi na ulemavu ili nao waweze kujiendeleza kimaisha kama watu wengine," alisema Maangi.
Maangi alisema kuwa serikali ya Kaunti ya Kisii imetenga shillingi million 15 ambazo zitatumika kuwasaidia wanaoishi na ulemavu huku akisema kuwa bunge la kaunti linastahili kupitisha mswaada wa jinsi pesa hizo zitakavyotumika kuwasaidia wanaoishi na ulemavu.
Aidha, Maangi aliomba wasimamizi wa shule kuhakikisha kuwa watoto wanoishi na ulemavu haswa mazeruzeru wanapata masomo kama wengine.
Akisema kuwa wanao wadhulumu watoto hao wachukuliwe hatua ya kisheria kwa sababau ulemavu si kizuizi cha mtu kuendelea na masomo au kujumuika na wenzake.
Kwingineko, amewaomba wahisani wema kujitolea ili kushirikiana na serikali ya kaunti kuwasaidia wanaoishi na ulemavu ili nao waweze kujiendeleza katika shughuli za kila siku.
“Naomba wahisani wema kujitokeza na kushirikina ili tuweze kuwasaidia wenzetu," alisema Maangi.