Serikali imetakiwa kuwapa nafasi za ajira mabaharia waliohitimu ili kusaidia katika kukabiliana na majanga katika maeneo ya fuo za Bahari Hindi.

Share news tips with us here at Hivisasa

Mwenyekiti wa Chama cha Mabaharia kanda ya Afrika mashariki na kati Daud Hajj amesema kuwa mabaharia wengi humu nchini na hususan katika eneo la Pwani wamefuzu kwenye sekta hiyo lakini bado serikali haijawatambua.

Akiongea wakati wa kuzinduliwa kwa mashua kutoka kwa Benki ya Dunia itakayotumika katika kukabiliana na majanga baharini katika eneo la Likoni siku ya Jumatano, Hajj alisema kuwa kuna umuhimu mkubwa wa ajira kutolewa kwa watu waliohitimu kwenye taaluma hiyo.

Hajj amependekeza Halmashauri ya Ubaharia nchini KMA, kuwashirikisha mabaharia katika meli zinazoingia humu nchini na kuelekea mataifa ya magharibi kama njia moja wapo ya kuimarisha usalama.

"Sisi kama mabaharia tunatambua kuwa serikali imetutenga lakini twaomba ituhusishe katika maswala ya ubaharia na kututengea nafasi za ajira ili kuhakikisha kuwa maswala ya usalama wa baharini unaimarishwa kikamilifu,” alisema Hajj.