Afisa Mratibu wa Bonde la Ufa Wanyama Musiambo amewahimiza machifu katika eneo lake kutoa funzo kutoka kwa ghadhabu aliyopewa naibu chifu wa eneo la Mawingu Joseph Wycliffe Rotich baada ya kunaswa akiwa mlevi siku ambayo rais Uhuru Kenyatta alikuwa akizuru eneo la Nakuru wiki iliyopita.
Musiambo akitangaza rasmi kufutwa kazi kwa chifu Rotich siku ya jumatano jijini Nakuru kufuatia tendo hilo amewaonya machifu kujitenga na unywaji wa pombe kwani ni njia moja ya kuwapotosha wananchi na kumakinika katika kupigana vita dhidi ya pombe hiyo haramu.
"Ni jambo la kusikitisha kuona kiongozi kama chifu akikunywa pombe hadharani bila aibu. Ninachukua fursa hii kukashifu kabisa tendo hili maanake ndilo linalochangia kuongezeka kwa biashara hii haramu. Iwapo machifu na manaibu wao kote nchini watajitolea na kuacha kujihusisha na unywaji pombe , basi hakuna sehemu tutashuhudia pombe tena," Musiambo alielezea.
Kando na machifu, Musiambo pia amewaonya viongozi wengine wakuu serikalini kuwa watachukuliwa hatua ifaayo iwapo watapatikana kujihushisha na biashara hiyo huku akiomba ushirikiano kutoka pande zote ili kukabiliana na janga hilo.
"Tutaendelea kufuata sheria jinsi ipasavyo na kuchukua hatua madhubutu ya kupeleka kortini yeyote atakayepatikana kujihusisha na biashara ya pombe. Hata viongozi wakuu serikalini hawatoponea iwapo watapatikana" Musiambo aliongezea.