Kamishna mkuu wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed amewataka machifu kuanza uchunguzi katika maeneo wanayohudumu ili kuwatambua wahusika wakuu wa uhalifu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Akizungumza kwenye mkutano wake wa kwanza na washikadau mbalimbali wa idara ya usalama ikiwemo machifu, Maalim alisema kuwa machifu watakuwa na jukumu kubwa ikilinganishwa na hapo awali, kwani watalazimika kuwasilisha ripoti ya usalama mara kwa mara katika afisi za wakuu wa usalama katika kaunti ndogo za Mombasa.

Kamishna huyo alisema kuwa kuibuka kwa makundi yanayotekeleza uhalifu maeneo mbalimbali ya mji wa Mombasa kunatokana na baadhi ya viongozi kukosa kuripoti visa viovu vinavyotekelezwa na vijjana wanaoaminika kuwa wahalifu.

Maalim alitaja Kisauni na Likoni kama maeneo yanayokubwa na visa vya uhalifu kwa kiasi kikubwa.

“Hakuna eneo linaloweza kuinuka kiuchumi iwapo usalama unazidi kudorora kwa kiasi kinachowatia wenyeji wasiwasi,” alisema Maalim.

Aidha, amesema kwamba tayari serikali kuu imejitolea kuimarisha usalama katika eneo hilo, kwa kuwa kila kituo cha polisi kilipewa gari ambazo ziliratibiwa kuwahudumia wananchi saa ishirini na nne.

Hata hivyo, amewaonya vijana wanaojiunga na makundi yanayowahangaisha wananchi kwa kusema kwamba uongozi wake hautasita kuwachukulia hatua.