Share news tips with us here at Hivisasa

Kamishna wa Kaunti ya Nyamira Josphine Onunga, ameahidi kuwapokeza machifu na manaibu wao pikipiki.

Machifu hao watatumia pikipiki hizo kutembelea sehemu mbalimbali katika maeneo yao yakuhudumu ili kuimarisha utoaji huduma.

Akihutubu kwenye hafla yakusherehekea siku ya Jamhuri kwenye uwanja wa michezo wa Nyamaiya siku ya Jumamosi, Onunga alisema hivi karibuni maafisa hao wa utawala watapokezwa pikipiki na serikali ya kitaifa kama njia mojawapo yakuimarisha utoaji huduma kwa wananchi.

"Tuna mipango yakuwapokeza machifu na manaibu wao pikipiki ili iwe rahisi kwao kuzuru maeneo mbalimbali katika sehemu zao za utawala, kuwawezesha kuwahudumia wananchi kwa urahisi," alisema Onunga.

Onunga aidha aliwahimiza wakazi wa kaunti hiyo kuwa waangalifu na kuripoti kwa polisi watu wanaoshukiwa kuwa tishio kwa usalama wao, hasa msimu huu wa likizo za krismasi.

Onunga aidha aliwarai wakazi kushirikiana na vyombo vya usalama ili kuimarisha usalama wao.

"Huu ni msimu wa likizo ya krismasi ulio na shughuli nyingi na kutokana na hili, watu huenda wakajihusisha na visa vya uhalifu. Himizo langu kwenu ni kuwa muwe macho na kutoa ripoti kwa maafisa wa polisi kuhusu watu mnaowashuku kuwa huenda wakawa tishio la usalama wenu," alisema Onunga.