Mwakilishi wa wanawake katika Kaunti ya Nyamira Alice Chae amewaomba maafisa wa utawala kujitokeza kuwalinda wanawake dhidi ya dhuluma za kijinsia.
Akihutubia wakazi kwenye kijiji cha Ritibo siku ya Jumapili, Chae alidai kuwa watu wanaowadhulumu wanawake huepuka kuadhibiwa kutokana na machifu na manaibu wao kutoshirikiana kukabili visa kama hivyo.
"Visa vya kudhulimiwa kwa wasichana wadogo kimapenzi na kuchapwa kwa kina mama vimekuwa vikishuhudiwa bila ya hatua kuchukuliwa kwa kuwa machifu na manaibu wao huwakinga washukiwa,” alisema Chae.
Chae aidha aliwaonya machifu dhidi ya kuwakinga washukiwa wa dhuluma za kijinsia akisema kuwa atashirikiana na washikadau kuhakikisha kuwa haki za wanawake zinalindwa, huku akisisitiza kuwa machifu ndio wanastahili kuwalinda wanawake kutokana na dhuluma za kijinsia.
"Ni jambo lakushangaza kwamba baadhi ya machifu huwakinga washukiwa wanao wadhulumu wanawake na kwasababu swala hili ni kama donda sugu, nimeamua kuwashirikisha washikadau kuhakikisha kuwa wanawake wanapata haki zao. Machifu wanastahili kuwalinda kina mama dhidi ya dhuluma kwa kuwa wao ndio wanaoishi karibu nao," alisema Chae.