Machifu na manaibu wao katika Kaunti ya Mombasa wametakiwa kuanza msako wa watoto ambao hawaendi shuleni.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Akizungumza mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Kamishna wa Kaunti ya Mombasa Maalim Mohamed, aliwataka viongozi hao wa utawala kuhakikisha kuwa hakuna mtoto anayebaki nyumbani pasi kutopata elimu.

Maalim alisema kuwa serikali imejitahidi kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu bila malipo katika shule zote za umma nchini, ili kila mtoto apate nafasi ya kujiendeleza maishani.

“Maafisa wa utawala wataanzisha oparesheni rudi shule katika kila eneo, ambapo wazazi wa watoto watakaopatikana wakikaa nyumbani bila kuenda shuleni, watachukuliwa hatua za kisheria,” alisema Maalim.

Maalim alisema kuwa hatua ya kutokwenda shule kwa baadhi ya watoto imechangia pakubwa visa vya uhalifu vinavyotekelezwa na vijana wenye umri mdogo, na kutatiza usalama wa kaunti.