Machifu na manaibu wao wa wadi ya Magenche iliyoko eneo bunge la Bomachoge Borabu kaunti ya Kisii wameombwa kuwachunguza wezi wa ng’ombe ambao wanaendelea na wizi huo katika eneo hilo.
Akizungumza siku ya Jumatatu katika eneo la Kiabugesi, mwakiliishi wa wadi Timothy Okiomeri Ogugu akiwa katika hafla ya kutembelea miradi yake ya maendeleo, aliwaomba machifu kufanya uchungunzi wa kina na kujua wanaotekeleza wizi huo wa ng’ombe.
Hii ni baada ya ng’ombe watatu kuibwa katika eneo la Kiabinyinyi usiku wa kuamkia jana.
Wezi hao hawakufanikiwa baadaa ya kufumaniwa na wakaazi na kutoroka huku wakiwaacha ng’ombe hao njiani jambo ambalo halikumfurahisha mwakilishi huyo.
Ogugu aliwaomba wakaazi wote wa eneo hilo pamoja na machifu kushirikiana pamoja kuzuia wizi wa aina hiyo.
“Tukishirikiana sisi sote na tuwe na umoja, wizi wa ngombe katika eneo hili hautaendelea kamwe. Naomba tushikane mikono tupambane na wizi huu ili tusishuhudie wizi wa aina hii tena katika eneo letu,” alisema Ogugu.
Mwakilishi huyo alitembelea miradi yake ya maendeleo katika eneo la Moteiribe, Mobirona, Kiabugesi na sehemu zingine.
Kwa upande mwingine wakaazi wa eneo hilo walimwomba mwakilishi kufanya maendeleo zaidi katika eneo hilo huku wakimwomba kupea mradi wa maji kipao mbele.
“Huwa tunasumbuka na maji katika eneo hili na tunamwomba mwakilishi wetu kutuwekea mradi wa maji kila sehemu kama njia ya kutupungunzia mzigo hasa sisi akina mama,” alisema Alice Omariba, mkaazi wa eneo hilo la Magenche.