Machifu wa lokesheni ya Kegati na ile ya Nyanko katika eneo bunge la Nyaribari Chache kaunti ya kisii wamepongezwa kwa msimamo wao mkalii kuhusu utumizi wa pombe haramu katika eneo hilo.
Hii ni baada ya kubainika kuwa lokesheni hizo zilikuwa miongoni mwa lokesheni ambazo zilikuwa na kiwango kikubwa cha upikaji wa pombe haramu, na viongozi hao wakahusika pakubwa katika uharibifu wa kinywaji hicho. .
Akizungumza siku ya Jumapili mjini Kisii, Mwenyekiti wa chama cha kupambana na dawa za kulevya katika Kaunti ya Kisii ambaye pia ni Mchungaji wa Chuo Kikuu cha Kisii kasisi Lawrence Nyaanga aliomba machifu wote kuwa na ushirikiano kumaliza pombe hiyo haramu, huku akipongeza machifu wa Kegati na Nyanko kwa kupambana na pombe hiyo.
Kulingana naye, ushirikiano huleta matunda mema kwa kumaliza pombe hiyo haramu, na kuomba machifu wa lokesheni zingine kuongeza motisha ya kumaliza upikaji wa pombe hiyo.
“Pombe imekuwa ikiathiri idadi kubwa ya vijana ambao hubugia pombe hiyo lakini ninaomba pombe hiyo kutopikwa popote,” alisema Nyaanga
“Naomba machifu wote katika sehemu wanazowakilisha kuhakikisha hakuna pombe haramu inapikwa katika sehemu hizo na ninapongeza chifu wa lokesheni ya Kegati na ile ya Nyanko kwa kuhakikisha pombe imekomeshwa kupikwa,” aliongeza Nyaanga.
Picha: Kasisi Lawrence Nyaanga. Amepongeza Machifu wa lokesheni ya Kegati na lokesheni ya Nyanko katika juhudi zao za kupigana na pombe haramu. Maktaba