Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Machifu na manaibu wao katika eneo la Bahati wameshutumiwa kwa kuwakinga wezi wa miti na wapasuaji haramu wa mbao katika msitu wa Bahati.

Naibu afisa msimamizi wa msitu wa Bahati Tom Odongo amesema kuwa baadhi ya machifu wanawajua watu wanaoiba miti kutoka msitu huo lakini hawataki kuwachukulia hatua za kisheria.

Odongo amesema kuwa kuna machifu ambao huwaruhusu watu hao kuingia msituni kuiba miti baada yao kupewa hongo.

Akizungumza wakati wa oparesheni ya kutafuta miti iliyoibwa kutoka msitu huo katika mtaa wa Kabatini Jumatatu, Odongo alisema kuwa licha ya maafisa wa kulinda misitu kutaka kushirikiana na machifu kuangamiza wizi wa miti katika msitu huo, juhudi hizo zimeambulia patupu.

“Tumekuwa na shida kidogo kati ya maafisa wetu na machifu ambao hawataki kuwataja wezi wa miti na kuwakamata.Wengine wanajulikana, lakini machifu wanawakinga kwa sababu wanapokea kitu kidogo kutoka kwao na hilo lazima ikome kama tunataka kuulinda msitu huu usiharibiwe,” Odongo alisema.

Aidha, afisa huyo alisema kuwa miti inayoibwa kutoka msitu huo hufichwa katika boma zilizo karibu kabla ya kusafirishwa nyakati za usiku na kuuzwa.

“Hii miti ikikatwa inafichwa kwa maboma hapa kando ya msitu na watu wa kununua wanakujia usiku na hilo machifu wanajua na hawataki kuchukua hatua,” aliongeza.

Aliwataka wakazi wa eneo hilo kushirikiana nao katika kulinda msitu huo kwa kuwaripoti watu wanaowashuku kuhusika na wizi wa miti msituni humo.