Wavulana wengi baada ya masomo ya msingi hukosa kuenda kujiunga na shule za upili na badala yake kujiunga katika kazi ya kuchimba mawe katika eneo la Katine katika kaunti ndogo ya Tala kaunti ya Machakos.
Hii ni kulingana na Mwenyekiti wa maendeleo ya wanawake katika kaunti ndogo ya Matungulu Victoria Mulalya.
Mulalya, akizungumza na wanahabari katika afisi yake eneo la Kisukioni siku ya Ijumaa alisema kuwa ana hofu kuwa maisha ya baadaye ya watoto hawa huenda yakakumbwa na ugumu kutokana na wao kutamani pesa kidogo za machimbo ya mawe bila kujua umuhimu was masomo maishani.
Aidha, Mulalya aliongezea kuwa kazi ya kuchimba mawe ni ngumu mno na haifai kupewa watoto wa umri mdogo kwani hio ni kazi ya sulubu, na kuongeza kuwa ni jambo la kusikitisha kuona vijana wadogo wakifanya kazi hii.
Alitaka wanaoajiri vijana hawa wadogo katika eneo hilo kuchukuliwa hatua za kisheria ili watoto waweze kusoma.
"Machimbo ya mawe ya Katine yanatupotezea watoto, wavulana wengi wameacha shule ili kuajiriwa katika machimbo haya bila kujua kuwa wanahatarisha maisha yao ya baadaye", alisema Mulalya.
Vile vile, aliwaomba wazazi kuhakikisha kuwa watoto wao wanasoma kwa kuwalipia karo na pia kuwahimiza kutilia masomo maanani.