Mwanaharakati wa haki za kibidamu Benard Atuya amemtaka gavana wa kaunti ya Nyamira John Nyagarama kuchunguza madai ya hospitali ndogo ya Ekerenyo kuwapikia wagonjwa chakula kibovu. 

Share news tips with us here at Hivisasa

Kwenye mahojiano na wanahabari mjini Nyamira siku ya Jumanne, Atuya alisema kuwa kwa muda usimamizi wa hospitali hiyo imekuwa ikiwapa wagonjwa maharagwe bila ugali na hata pia wakati mwingine wagonjwa kupikiwa ugali kutoka kwa unga ulioharibika.

"Kuna siku niliposhuhudia wagonjwa wakipikiwa maharagwe pekee kama chakula cha jioni, na hata pia wakati mwingine wao hupikiwa ugali wa unga ambao tayari umeharibika, suala ambalo ni lakushangaza sana. Ni ombi langu kwa gavana kulichunguza suala hilo," alisema Atuya.

Atuya aidha alisema kuwa sharti maafisa wakuu wa hospitali hiyo wawajibikie pesa zinazotumwa kufadhili mahitaji ya hospitali hiyo, huku akitishia kufanyika maandamano ya wananchi iwapo hali hatarekebishwa.

"Ikiwa pesa zimetuma kwenye hospitali zetu ili kufadhili miradi na mahitaji mbalimbali sharti wasimamizi wa hospitali hiyo wawajibikie matumizi ya pesa hizo na hali kurekebishwa kabla yetu wananchi kuandamana," aliongezea Atuya.