Maafisa wakuu wa polisi katika kituo cha polisi cha Central mjini Nakuru, wamepinga madai yanayosambazwa na baadhi ya wenyeji wa kaunti hii kwamba kumezuka wimbi jipya la uhalifu wa kuteka nyara magari.
Wakaazi waliotoa taarifa kwa mwandishi huyu mjini Nakuru Jumanne, walisema jumla ya magari matano yametekwa nyara katikati ya mji mwezi huu wa Disemba pekee, na watu ambao wana bunduki na kuvalia sare kama za polisi.
Hata hivyo katika mahojiano ya moja kwa moja na mwandishi huyu ofisini mwake, kaimu mkuu wa polisi (OCPD) Musa M. Kongoli, alikanusha madai hayo akiyataja ‘propaganda za watu wasiopendelea kazi nzuri ya polisi’.
Kulingana na mkuu huyo, utekaji nyara wa magari na malori ya kusafirisha mizigo umepungua kutokana na mikakati mipya ya kiusalama ambayo imewekwa.
“Tuna mpangilio mzuri sana wa kuhakikisha tunaelewa kila kinachofanyika, tukisaidiana na raia wema wanaotupasha habari. Kila asubuhi tuna mkutano hapa kituoni, kuangalia jinsi matokeo ya jana yalikuwa, na kisha tunapanga ya siku hiyo. Pia tuna kikosi spesheli ambacho tumeteua na kazi yake ni kuhakikisha wanakimbia pahali usaidizi wa polisi unatakikana,” Musa alisema.
Hata hivyo bwana Musa alitoa wito kwa wanahabari kufanya kazi yao kwa namna ya kusaidia raia, na wala sio kubomoa jamii.
"Kulingana na rekodi zetu, visa kadhaa vya utekaji nyara viliripotiwa mwezi Novemba na Oktoba, na wanaosema mwezi huu utekaji nyara umefanyika wanapaswa kutuletea ripoti hiyo kusudi tufanye uchunguzi," mkuu huyo aliongeza.