Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Viongozi wa chama cha madaktari wa miti shamba humu nchini maarufu kama NATHEPA wametoa wito kwa serikali na idara ya usalama kuendeleza oparesheni dhidi ya waganga bandia wanaondelea kuwalaghai wakenya.

Mwenyekiti wa chama hicho eneo la Pwani ambaye pia ni naibu mwenyekiti wa kitaifa Mohamed Kitsao alisema kuwa kuna madaktari bandia wanaotapeli wakenya kwa kudai kutibu maradhi tofauti ilihali ni uongo.

Akizungumza na mwanahabari huyu siku ya Ijumaa katika makao makuu ya chama hicho, Kitsao alisema kuwa kufikia mwezi Februari mwakani, kwa ushirikiano na maafisa wa utawala, wataanzisha oparesheni ya kuwasaka wahudumu wote bandia wanaoendesha shughuli hiyo ilihali hawajajisajili na chama hicho.

Wakati huo huo, chama hicho kimeunga mkono kauli ya kamishna wa kaunti ya Mombasa Nelson Marwa ya kuondolewa kwa vibao vyote vya waganga mjini Mombasa, huku mwenyekiti huyo akisema kuwa kufikia sasa, zaidi ya vibao 37 vimeng’olewa kwa ushirikiano na maafisa wa utawala.