Share news tips with us here at Hivisasa

Idara ya Trafiki katika Kaunti ya Nakuru imewataka madereva kuwa waangalifu barabarani haswaa wakati huu ambapo sehemu nyingi za nchi zinashuhudia mvua kubwa.

Kupitia kwa afisa mkuu wa trafiki katika eneo la Bonde la Ufa Mary Omari, idara hiyo ya trafiki imesema mvua hiyo imeripotiwa kusababisha ukungu barabarani kwenye sehemu zingine za nchi kama vile Kinungi, hali ambayo husababisha madereva wanaoendesha magari yao kwenye sehemu hizo kutatizika.

Kwenye mahojiano na mwandishi huyu afisini mwake mjini Nakuru siku ya Ijumaa, Bi Omari aliwataka madereva kutoendesha magari yao kwa kasi, akiashiria kuwa ajali nyingi za barabarani ambazo husababisha vifo hutokana na madereva wanaoendesha magari yao kwa kasi.

Isitoshe, amewataka madereva pia kuwa waangalifu haswaa wanapoendesha magari yao katika barabara ambazo hawajazoea.

“Wakati ambapo kuna mvua , huwa ni vigumu kwa madereva kuona barabara vizuri. Maeneo ya Kinungi na Timboroa huwa na ukungu, na kutokana na hilo, ni vigumu kuona barabara kwa urahisi. Kutokana na hilo, ningependa kuwasihi madereva kuwa waangalifu kwa kuwa kunaponyesha, ni vigumu hata kukanyaga breki kwani barabara huteleza,” alisema Omari.

Wakati huo huo, ameipongeza serikali kwa kumaliza pombe haramu nchini, hatua aliyosema imepelekea idadi ya ajali za barabarani kupungua.

Omari alisema kwamba idadi kubwa ya ajali zilizoshuhudiwa hapo awali zilitokana na wapita njia waliobugia vileo kupindukia, hatua ambayo iliwapelekea kuvuka barabara kiholela na hivyo kugongwa na magari.

“Ningependa kushuruku serikali kwa sababu ukiangalia mjini Nakuru, idadi ya ajali zilizokuwa zikitokea hapo awali zilikuwa zile za wapita njia. Kwa wikendi moja ungepeta wapita njia kumi wamegongwa. Hata hivyo, tangu serikali ilipoanzisha oparesheni ya kukabiliana na pombe haramu, idadi ya ajali imepungua,” alisema Omari.