Share news tips with us here at Hivisasa

Madereva wa magari ya uchukuzi wa umma wameonywa dhidi ya kubadili njia zilizosajiliwa na wamiliki wa magari hayo kwa misingi ya kutafuta pesa za haraka.

Haya ni kwa mujibu wa mshirikishi wa wamiliki wa matatu ukanda wa Pwani Salim Mbarak akidokeza kuwa baadhi ya madereva wa matatu wamekuwa na tabia ya kubadili njia zao haswa wakati huu wa msimu wa sherehe wakitafuta abiria zaidi jambo ambalo amesema kuwa ni kinyume na sheria.

“Madereva wanaobadili njia zao walizosajiliwa nazo kwa kutaka kupata pesa za haraka kutokana na abiria katika njia hizo,wajue kwamba wanakiuka sheria na hatua zitachukuliwa dhidi yao” alisema Salim.

Salim ameongeza kuwa hatua hiyo ya madereva kubadilisha njia zao huchangia pakbwa katika msongamano wa magari katika barabara ikizingatiwa kuwa idadi inayotumia njia au barabara hizo inaongezeka maradufu.

Vile vile amewataka maafisa wa kitengo cha trafiki pamoja na wale wa halmashauri ya uchukuzi na usalama nchini yaani National Transport and Safety Authority (NTSA) kuwa chonjo wakati wanapotekeleza majukumu yao ili kukabiliana na wale wote watakao kiuka sheria za barabarani.

Sekta ya uchukuzi imeonekana kuimarika pakubwa haswa katika msimu huu wa likizo na shamra shamra za krismasi huku idadi kubwa ya wakaazi kutoka maeneo tofauti za humu nchini wakisafiri ili kujumuika na jamaa na familia wakati huu wa sherehe.

Hata hivyo mshirikishi huyo alisisitizia madereva kutotumia ulevi wa aina yoyote kwa kisingizio cha kujiweka macho wakati wanapoendesha magari hatua ambayo aloitaja kama miongoni mwa vyanzo vya kusababisha ajali.