Madereva wa tuktuk wanaowabeba abiria kupita kiasi mjini Mombasa wameonywa dhidi ya tabia hiyo hatari.

Do you have a lead on a newsworthy story? Share news tips with us here at Hivisasa!

Inadaiwa wahudumu hao wamekuwa wakiwabeba abiria wengi kwa pamoja jambo linalotajwa kuchangia kushuhudiwa kwa ajali nyingi katika eneo hilo.

Akizungumza na mwandishi huyu siku ya Jumatano afisini mwake, mwenyekiti wa Muungano wa Wamiliki wa Tuktuk Mombasa Obedi Muruli, alisema madereva wengi wanaokiuka agizo hilo ni wale wanaohudumu eneo la feri.

“Madereva wa feri ndio wenye tabia hiyo ambapo utapata mtu anabeba zaidi ya watu wanne huku wengine wakibeba hata watu wasaba,” alisema Muruli.

Muruli alidokeza kuwa idadi rasmi ambayo tuktuk inafaa kubeba ni watu watatu na kama itabidi kuongeza zaidi, pengine idadi hiyo ifike nne.

Wakati huo huo, aliwalaumu maafisa wa trafiki wanaohudumu barabarani kwa kulifumbia macho swala hilo.

Mwenyekiti huyo alisisitiza kwamba kulingana na sheria, abiria waliozidi hawawezi kulipiwa bima ajali inapotokea kwani hawatambuliwi kama abiria halali.

“Tuktuk yenyewe imeandikwa kwamba inafaa kubeba watu watatu lakini madereva wameigeuza kuwa kama matatu na ajali inapotokea, abiria wote hawawezi wakafidiwa,” aliongeza Muruli.

Usafiri wa tuktuk ni maarufu sana mjini Mombasa hasa katika maeneo ya mjini.