Maafisa wa trafiki mjini Molo wanamzuilia dereva wa basi la shule kwa kosa la kubeba abiria kupita kiasi.
Basi hilo ambalo linamilikiwa na Kipsigis Teachers Training College, lilikuwa limebeba wanafunzi 70 badala ya kiwango chake cha wasafiri 51.
Wasafiri hao wamesema waliabiri basi hilo kutoka Kericho, ili kuweza kuhudhuria kongamano la makanisa linalofanyika wilayani Kuresoi kabla, ya kukamatwa na maafisa wa trafiki katika eneo la Mau Summit.
Kamanda wa trafiki wilayani Molo Richard Masinde amesema basi hilo alilokamata, lilikuwa linahatarisha maisha ya abiria hao, ambao wengi ni wanafunzi.
Masinde amesema msimu huu wa kirisimasi huwa na wasafiri wengi, huku madereva wakikiuka sheria za trafiki ili kuzoa fedha zaidi.
Amewauliza wasafiri kuteta iwapo wahudumu wa magari ya usafiri ya umma yanabeba abiria kupita kiasi, akisema ni sharti abiria wafunge mishipi ya usalama wanaposafiri.
Dereva huyo atafikishwa mahakamani hapo kesho.
Wakati huo huo, mhudumu wa pikipiki na mteja wake wanapokea matibabu katika hospitali ya wilaya Molo, baada ya kuhusika kwenye ajali.
Walioshuhudia ajali hiyo wamesema pikipiki hiyo iligongana na gari la kibinafsi kwenye barabara ya Total –Mau summit.