Madereva na utingo wao katika steji ya Keroka, Kaunti ya Nyamira wameonywa dhidi ya kuvunja sheria za barabarani.
Madereva hao walionywa kuwa watatiwa mbaroni na kuchukuliwa hatua kali ya kisheria.
Wito huo umetolewa na mkuu wa polisi katika kaunti ya Nyamira Abraham Ndewa ambaye aliagiza madereva na utingo wao kuwabeba abiria katika kituo cha magari cha Keroka wala si kuwabebea abiria kandokando mwa barabara ya mji wa keroka.
Haya yanajiri baada ya steji mpya kujengwa na kufunguliwa katika mji wa Keroka ambapo wameagizwa kukitumika kupanga abiria.
Akiongea siku ya Jumatatu katika steji hiyo ya Keroka, Ndewa alisema sharti madereva na utingo wao kufuata sheria jinsi ilivyo na ili kuepuka kufikishwa kotini kujibu mashtaka ya kuvunja sheria za barabarani.
“Sisi maafisa wa polisi hatutakuwa na maneno mengi ikiwa madereva wanafuata sheria. Naomba sheria za barabarani zifuatwe. Abiria wote wawe wakipanda gari katika steji mpya ya Keroka maana kituo hiki kilijengwa ili abiria wawe wanapandia hapo wala si kandokando mwa barabara," alisema Ndewa.
Kituo hicho cha magari kilifunguliwa wiki mbili zilizopita huku watu wote hasa madereva wakiagizwa kukitumika.