Madereva wa mabasi kwenye vituo vya kuengesha magari katika eneo la Mwembe Tayari wameunga mkono pendekezo la kutumia mabomba yenye upana wa inchi ishrini kusafirisha mafuta ili kupunguza msongamano wa magari unaoshuhudiwa mara kwa mara katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.
Wakizungumza siku ya Jumatatu katika vituo vyao, madereva hao walisema kuwa sekta ya uchukuzi itapata afueni kwa kuwa hatua hiyo itapunguza msongamano wa magari katika barabara kuu ya Mombasa-Nairobi.
Walisema kuwa kuondolewa kwa malori elfu nne kama inavyodhamiriwa na kampuni ya kusafirisha mafuta (KPP) katika barabara hiyo kutatoa nafasi kwa mabasi yanayowasafirisha abiria kuweza kufika jijini Nairobi kwa muda ufaao.
Akilinganisha hali ya usafiri hapo awali katika eneo la Taru, Ahmed Swaleh, dereva wa kampuni ya Tahmed Coach alisema kuwa kuna wakati iliwalazimu kulala katika eneo hilo kutokana na msongamano mkubwa uliosababishwa na ukarabati wa barabara hiyo.
Swaleh alielekeza kidole cha lawama kwa madereva wa malori aina ya trela kwa kusema kuwa huwa wajeuri wanapofika kwenye msongamano.
Kauli ya Swale iliungwa mkono na dereva mwenza wa kampuni ya TSS Mwangi Abdallah, ambaye alisema kuwa wengi wa abiria wamekuwa wakilalamikia milolongo mirefu ya magari kuanzia kwenye daraja la kupima uzito la Mariakani hadi eneo la Taru.
Kulingana na kaimu mkurugenzi mkuu wa kampuni ya kusafirisha mafuta Joe Sang’ni zabuni hiyo ya kutengeneza mabomba hayo ilipewa kampuni ya kimataifa ya Zakhem mnomo mwaka wa 2014.