Madereva wanaoendesha magari katika kaunti ya Kisii wameonywa vikali dhidi ya kuendesha magari wakiwa walevi kupita kiasi kuwa watanyang'anywa leseni zao za kuendesha magari barabarani.
Onyo hilo limetolewa baada ya madereva 16 mjini Kisii kutiwa mbaroni na maafisa wa traffiki mnamo tarehe 25 Disemba siku ya krismasi walipofumaniwa wafanyi biashara zao za uchukuzi wakiwa walevi.
Akizungumza siku ya Jumatatu mjini Kisii afisa mkuu wa kitengo cha trafiki wilayani Kisii ya kati Erick Gitinji alisema dereva yeyote atafumaniwa akiendesha gari akiwa mlevi atakamatwa na kunyanganywa leseni ya kuendesha magari barabarani ili kuwa funzo kwa wengine.
Kulingana naye msimu huu wa sherehe nyingi haswa za kukaribisha mwaka mpya wakati idadi nyingi ya wakaazi wanakutana na wenzao nyumbani madereva wanastahili kuendesha magari wakiwa waangalifu ili kuzuia visa vya ajali vinavyofanyika kila mara na kugharimu maisha ya watu.
“Naomba kila dereva azingatie sheria za barabarani na kuwa mwangalifu ili kupunguza visa vya ajali barabarani,” alisema Erick Gitinji.
“Yeyote atakayefumaniwa akiendesha gari akiwa mlevi atakamatwa na kunyang'anywa leseni ya uendeshaji magarai barabarani,” aliongeza Gitinji.
Gitinji alisema mmoja wa madereva waliotiwa mbaroni tarehe 25 Disemba atanyang'anywa leseni yake kwani yeye alikuwa mlevi kwa kiwango cha 1.04 kupita kiwango kile wanachokubaliwa cha 0.1.
Aidha, afisa huyo aliwaomba madeva na utingo wao kuwa na heshima wanapofanya biashara zao za uchukuzi kwani wengi wa wakaazi hutembea na wanao katika msimu huu wa sherehe.