Idara ya usalama katika eneo la Likoni, Kaunti ya Mombasa, imeanza mikakati ya kulinda maduka ya M-Pesa kama njia moja ya kupunguza visa vya uhalifu.

Share news tips with us here at Hivisasa

Idara hiyo imesema hivi karibuni itafanya kikao na wamiliki wa maduka hayo, ili kufanya makubaliano ya muda mwafaka ambao wahudumu hao wanafaa kufanya kazi.

Akizungmza kwenye mkutano wa usalama siku ya Jumatatu katika afisi za Likodep, Naibu kamishna wa Likoni Albert Kimanthi alisema kuwa ipo haja ya kuweka muda maalum wa kuhudumu, ili idara hiyo iweze kuwalinda ipasavyo.

“Kwanini wafanyabiashara wa M-Pesa wanahudumu hadi saa nne na wengine hata saa tano usiku? Tunataka kwanza tushikane na wadau tupange mikakati ili nasi pia iwe rahisi kuwalinda,” alisema Kimanthi.

Afisa huyo alisema imekuwa vigumu kwao kudhibiti visa vya uhalifu ambapo biashara hiyo inaonekana kulengwa zaidi, kwani hakuna muda maalum wa kufungua na kufunga biashara hiyo.

Kauli yake inajiri baada ya maduka kadhaa ya M-Pesa kuvamiwa na wahalifu na maelfu ya pesa kuibiwa.

Katika kisa cha hivi majuzi, mwanamke mmoja aliuawa kwa kupigwa risasi kabla majambazi kuiba pesa na kutoroka.