Pwani imebaki nyuma kimaendeleo kwa muda mrefu sana.
Wananchi wa sehemu hii wamekumbwa na mikosi mingi inayotokana na uongozi duni.
Taswira hii ya kuvunja moyo imefanya wanasiasa matapeli kuwatumia Wapwani kama vyombo vya kukamilisha ndoto zao. Ubinafsi huu ndio unaua uzalendo Pwani.
Wapwani hawastahili kuhongwa na serekali au kiongozi yeyote. Maendeleo ni haki ya kikatiba ya kila mwananchi bila kuzingatia mrengo wa kisiasa anaoegemea.
Demokrasia inatuelekeza jinsi ya kugawa raslimali ya taifa.
Ukija Pwani na uanze mradi wa kuwapa wananchi maji safi, hili lisiwe jambo la kupigia siasa isiyo na dhamana.
Barabara nzuri si jambo ambalo tunastahili kuongelea miaka nenda miaka rudi. Kuna sehemu humu nchini ambazo hazichangii kwa vyovyote vile katika ukuaji wa uchumi wa taifa letu ilhali barara zai ni za kupigiwa mfano Africa Mashariki.
Kwanini Pwani isiwe na miundo msingi kama hizo? Tuna watalii, madini, bandari na mengineyo.
Twajua watoto wetu wamepotoshwa na dawa za kulevya. Iwapo kiongozi atanasa walanguzi ama aanzishe kituo cha kurekebisha tabia, hili halifai kuwa shurutisho la kuwapa kura.
Aidha, ukahaba upo Pwani na jamii inalaani vitendo hivi. Ni jukumu lako kama kiongozi kushirikiana na jamii kung'oa gonjwa hili Pwani. Elimu pia sharti iimarishwe.
Mashamba, usalama, kazi na ukabila ni vitu viongozi wamekua wakivitumia kujipigia debe tangu tupate uhuru kutoka kwa mkoloni.
Ni uhuru kutoka kwa wakoloni kwa sababu uhuru kutoka kwa wazaliwa wa papa hapa Kenya haupo kikamilifu.
Vyeti vya umiliki wa mashamba ni haki ya wapwani. Usalama murua na kutovurugwa kwa misingi ya kabila ni haki ya kila Mkenya.
Kazi tunazoahidiwa kila siku zipeanwe na mazingira mema ya kujiajiri kibinafsi yatengenezwa na wanaohusika.
Maendeleo yasiwe mtego kwa wapwani. Yaletwe kulingana na ahadi za kampeni.