Shughuli za wakaazi wa mji wa Mombasa zinaendelea kutatizika kufuatia mvua kubwa inayoendelea kushuhudiwa katika eneo hilo.
Mafuriko yanayoshuhudiwa katika eneo hilo yanaathiri usafiri kwa kuziba barabara na pia kuleta tishio la mkurupuko wa magonjwa.
Wakaazi wengi wameilaumu serikali ya Kaunti ya Mombasa kwa kutowajibika katika juhudi zake za kutatua swala la mafuriko kwa kukarabati mabomba na mitaro ya kupitisha maji taka.
Wakaazi hao wamesema kuwa mafuriko hayo yamekuwa kizuizi katika harakati zao za kuendesha shughuli zao za kila siku.
Baadhi ya madereva waliozungumza na mwandishi huyu siku ya Ijumaa walilalamikia hali ya kukwama kwa magari yao, huku mengine yakiharibika.
Madereva hao waliitaka serikali ya kitaifa pamoja na ile ya kaunti kuangazia swala hilo na kukarabati barabara zilizo katika hali mbaya.
Madereva hao walisema kuwa barabara hizo mbovu huwafanya kupoteza muda mwingi barabarani, hali inayosababisha wateja wao kuchelewa kazini.
Hata hivyo, wakaazi hao wana matumaini kuwa serikali ya kaunti itajizatiti kuhakikisha kuwa tatizo hilo linatatuliwa kikamilifu