Hasara kubwa ilishuhudiwa katika kampuni moja ya kuhifadhi kemikali eneo la Shimanzi mjini Mombasa siku ya Alhamisi, baada ya moto kuzuka katika mabohari.
Moto huo ulizuka katika kampuni hiyo ya Solvochem Limited mwendo wa saa tisa jioni wakati wafanyikazi walipokuwa wakishukisha mizigo kutoka kwenye trela.
Akiongea na wanahabari katika eneo la tukio baada ya mkasa huo, OCPD wa Mombasa Martin Asin alisema kuwa trela tatu zilichomeka.
“Ni mkasa ambao umesababisha hatari kubwa. Trela tatu zimeweza kuchomeka lakini tunashukuru maafisa wetu kwa kushughulikia mkaso huo kwa dharura, kwani wamejitahidi sana,” alisema Asin.
Halmashauri ya Bandari KPA pamoja na ile ya viwanja vya ndege KAA wakishirikiana na kaunti ya Mombasa walifika eneo la tukio na kufaulu kudhibiti moto huo.
Afisa mkuu wa kukabiliana na dharura katika halmashauri ya KPA Geofrey Namadowa alisema kuwa walijitahidi kuzima moto huo kwa wakati ufaao lakini akaongeza kuwa wanaendelea na uchunguzi kubaini kiini hasa.
Hata hivyo, hakuna mtu aliyefariki kutokana na mkasa huo, wala hakukuwa na majeruhi kwani wafanyikazi walifaulu kukwepa baada ya tahathari kutolewa.
“Mimi nilikuwa naendela na kazi kama kawaida nikasikia wenzangu wananiambia nitoke haraka. Baadae ndio nikaona moshi ukitoka huku magari yakichomeka,” alisema mfanyikazi mmoja.