Dereva wa matatu aliyekamatwa kwa kuonyesha video chafu na kucheza mziki kwa sauti ya juu. Picha/Brian Otieno.

Share news tips with us here at Hivisasa

Polisi walimkamata dereva mmoja wa gari la abiria siku ya Jumatatu mjini Mombasa baada ya kupatikana kucheza mziki kwa sauti ya juu na pia kuonyesha video chafu.

Hatua hii inajiri baada ya kuwa na malalamiko kuzidi kutoka kwa viongozi wa kidini, wazazi pamoja na raia.

Matatu hiyo inayobeba abiria kutoka Mombasa kuelekea Mtwapa ilikuwa imepewa onyo na bodi ya kudhibiti filamu nchini.

Wiki jana dereva pamoja na kondakta wa matatu hiyo waliwafurusha abiria ambao walionekana wakilalamikia tabia hiyo.

Jason Murimi ambaye alikuwa miongoni mwa abiria waliofurushwa alisema kuwa alikuwa ameabiri gari akiwa na familia yake pamoja na mtoto wake wa miaka 10 wakati video chafu ilipokuwa ikionyeshwa ndani ya matatu hiyo.

“Nililalamika pamoja na abiria wenzangu lakini hatukusikizwa na baadaye tukaambiwa tushuke,” alisema Murimi.

Dereva huyo pamoja na kondakta wake walikamatwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Mtwapa.

Mkurugenzi mkuu wa bodi ya kudhibiti filamu nchini kanda ya Pwani Bonventure Kioko aliwataka maafisa wa polisi kuwa waangalifu sana barabarani.

“Huu ni mwanzo tu na hatutakuwa na mazungumzo tena kuhusiana na swala hili. Televisheni zote ndani ya magari zitaondolewa,” alisema Kioko.

Kioko aliongeza kuwa Matatu zinazowabeba abiria kutoka Mtwapa hadi Mombasa zitachunguzwa sana na wahudumu wake kuchukuliwa hatua iwapo watapatikana wakikiuka maadili mema.