Katibu Mkuu katika Wizara ya Ufugaji nchini Profesa Fred Segor amewaomba Magavana wote nchini kupatia mradi wa ufagaji wa ng’ombe wa maziwa kipao mbele ili kuimarisha uchumi wa taifa.
Akizungumza siku ya Alhamisi katika eneo la Itibo, Kaunti ya Nyamira alipotembelea wafugaji mbali mbali wa ng’ombe wa maziwa, Profesa Segor alisema Serikali Kuu ikishirikiana na shirika la EVAD iliona ni jambo la busara kushirikiana na Serikali za Kaunti ili kuimarisha ufugaji wa ng’ombe wa maziwa.
Serikali ya Kaunti ya Nyamira ilikabidhiwa Sh6 millioni kwa ufugaji huo na kaunti hiyo imeonekana kuendelea mbele zaidi kupitia ufugaji huo wa Ng’ombe wa maziwa.
“Tulianza ufugaji huu kote nchini tukiwa na ng’ombe wa maziwa millioni 1.4 na sasa ng’ombe hao wameongezeka hadi millioni 4.5 kote nchini. Tutaendelea zaidi ili viwango vya ufugaji wa ng’ombe viinuka na wafugaji kujiimarisha kibiashara,” alisema Profesa Segor.
Wakati uo huo, katibu huyo alitembelea eneo la Gesore, Kebirigo na Itibo ambapo wafugaji wa ng’ombe hao waliko.
Aidha, Naibu Gavana wa Kaunti ya Nyamira Amos Nyaribo aliyemkaribisha katibu huyo alisema kuwa ufugaji huo umekuwa wa maana sana hasa kwa kaunti hiyo tangu mradi huo uanzishwe.
“Tumenunua mitungi ya maji kwa kila Wadi ambayo itasaidia ng’ombe hao kupata maji kila wakati. Natarajia kuwa ufugaji huu wa ng’ombe wa maziwa utaenezwa kwa Wadi zingine ambazo zilibaki (ambazo ni 20) maanake tulianza na Wadi saba,” alisema Naibu Gavana Nyaribo.