Mwenyekiti wa baraza la magavana, Josephat Nanok. [Picha/nation.co.ke]
Baraza la magavana nchini limeitaka idara ya upelelezi na kwa ushirikiano na idara zigine za usalama kuhakikisha linafanya uchunguzi wa haraka kubaini kilichosababisha ajali ya barabara iliyogharimu maisha ya gavana wa Nyeri dakta Wahome Gakuru.
Mwenyektii wa baraza hilo Josphat Nanok amesema licha ya kwamba wameelezwa ilikuwa ajali ya barabarani wanataka kufahamu zaidi kilichopelekea ajali hiyo.
Wamesema ajali hiyo haifai kuchukuliwa tu kama ya kawaida hadi uchunguzi utakapofanywa.
Kufuatia kifo cha gavana Gakuru, naibu gavana wa Nyeri dakta Mutahi Kahiga sasa ndiye atakayehudumu kama gavana kwa muda uliosalia.
Tayari baraza la magavana limedhibitisha kupokea ushauri wa mabadiliko hayo, huku matayarisho ya kumuapisha Kahiga yakianzishwa rasmi.
Kulingana na katiba, naibu gavana anapaswa kuchukua hatamu ya uongozi wa kaunti iwapo nafasi ya gavana itaachwa wazi.
Hii ni mara ya pili kwa kaunti ya Nyeri kukumbwa na mkasa aina hiyo.
Mwezi February mwaka huu, aliyekuwa gavana kwa wakati huo Nderitu Gachagua aliaga dunia alipokuwa akipokea matibabu yake huko London.
Gachagua alifariki kutokana na ugonjwa wa saratani.