Magavana wamewaponda maafisa wa serikali kuu kwa madai ya kukusanya ushuru ambao unastahili kukusanywa na maafisa wa serikali za kaunti.

Share news tips with us here at Hivisasa

Wakiongozwa na gavana wa jimbo la Kakamega Wycliffe Oparanya, magavana hao walisema imekuwa vigumu kwa serikali za kaunti kukusanya kiwango cha ushuru kinachostahili, kutokana na kile wanachosema ni usumbufu wa maafisa wa serikali kuu.

“Sipendi kauli ambayo hutolewa na maafisa wa serikali kuu kwamba wamepeana pesa kwa serikali za kaunti. Wanapena hizo pesa kutoka wapi? Hizi ni pesa za walipa ushuru,” alisisitiza Oparanya.

Naye gavana wa jimbo la Meru Peter Munya alisema kuwa kiwango cha ukusanyaji ushuru humu nchini kutaimarika pakubwa, iwapo serikali ya kitaifa na zile za kaunti zitashirikiana katika mchakato wa ukusanyaji ushuru.

“Ukweli ni kwamba serikali za kaunti zinaendelea kukusanya kiwango kikubwa cha ushuru, zaidi ya ilivyokuwa chini ya mabaraza ya miji,” aliongeza gavana huyo wa Meru.

Wawili hao walisema hayo wakati wa kufungwa rasmi kwa kongamano la pili la baraza la magavana, lililoandaliwa kwenye ukumbi wa chuo cha leba cha Tom Mboya jijini Kisumu.

Kongamano hilo lililoanza siku ya Jumanne na kuhudhuriwa na wajumbe wapatao 6,000, lilikamilika rasmi Alhamisi jioni.

Hata hivyo, naibu wa rais William Ruto hakujitokeza kulifunga rasmi kongamano hilo, jinsi ilivyokuwa imeratibiwa hapo awali.