Share news tips with us here at Hivisasa

Mbunge wa Nyali, Hezron Awiti, ameshutumu tukio la hivi majuzi la kuuwawa kwa afisa mmoja wa polisi aliyepigwa risasi na genge la majambazi waliotoroka na bunduki yake.

Awiti alisema tukio hilo ni lakusikitisha na lazima maafisa wa polisi kuweka mikakati mwafaka ya kuimarisha usalama pamoja na kuliandama genge hilo kikamilifu, ili kusitsisha kushuhudiwa kwa visa vya kihalifu katika Kaunti ya Mombasa.

Akizungumza na wanahabari mjini Mombasa siku ya Alhamisi, Awiti alisema kwamba hatua ya kuwauwa maafisa wa polisi bila sababu zozote mwafaka linafaa kusitishwa mara moja na magenge ya kijambazi kuandamwa na kukabiliwa kikamilifu.

“Tunasikitika kuona afisa wa polisi akiuwawa na genge la majambazi na kisha kutoroka na bunduki yake. Hilo linafaa kudhibitiwa mara moja na genge hilo la majambazi kuandamwa na kukabiliwa ili kaunti iwe na usalama,” alisema Awiti.

Wakati huo huo aliyakashifu vikali mashirika ya kutetea haki za kibinadamu kwa kusalia kimya kinyume na hapo awali walipokuwa wakijitokeza na kukashifu vitendo vya mauaji akisema kwamba mashirika hayo huegemea upande mmoja na kutowajali maafisa wa usalama.

“Tunashangazwa na jinsi mashirika ya kijamii yalivyosalia kimya kwa sababu aliyeuwawa ni afisa wa polisi. Hilo sio jambo jema kwa sababu afisa wa polisi ana haki kama raia mwingine yule. Tunapigania haki za maafisa wetu ili pia nao watambulike kama raia wengine,” aliongeza Awiti.

Hata hivyo Idara ya usalama katika kaunti ya Mombasa imezidi kuwaagiza wahalifu waliyotekeleza kitendo hicho na kutoroka na bunduki ya fisa huyo aina ya G3 kurejesha bunduki hiyo mara moja la sivyo hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Tukio hilo la kuuwawa kwa afisa huyo wa polisi wiki iliyopita lilileta pamoja maafisa wa idara mbalimbali za polisi, viongozi wa kisiasa na wanaharakati wa kijamii kutafuta mbinu mbadala za kukabiliana na magenge ya kihalifu ili kuimarisha usalama kwa kaunti ya Mombasa.