Kitita cha zaidi ya shilingi milioni 55 kimetolewa na benki ya dunia kupitia shirika la utunzi wa mazingira kanda ya Ziwa Victoria (LVEMP) Kenya kwa minajili ya kujenga mahabara ya kisasa ya kutibu maji katika eneo la Nyalenda.

Share news tips with us here at Hivisasa

Haya ni kwa mjibu wa katibu mkuu katika wizara ya maji, mazingira na rasilimali asili Richard Lesiyampe, ambaye amesema shilingi milioni 18 zimetumiwa kwa ujenzi wa jumba hilo, huku milioni 33 zikitumiwa katika ununuzi wa vifaa vya mahabara.

Kwenye hotuba yake iliyosomwa na katibu wa kudumu kwenye wizara hiyo Julius Kandie wakati wa kuzindua rasmi mahabara hiyo, Lesiyampe alisema mahabara hiyo itatumika kuhakikisha kuwa wenyeji wanapata maji safi, na vile vile itatumiwa na taasisi za elimu kufanya utafiti.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutunza mahabara hiyo baada ile ya hapo awali kuteketezwa kufuatia machafuko ya ghasia za baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2007/2008.

Mahabara hiyo inatarajiwa kusaidia kuimarisha mazingira ya mji wa Kisumu, ulioko kando kando mwa ziwa hilo la Victoria.