Dereva wa tuktuk Samuel Mwangi ameelezea mahakama kuwa mfanyibiashara Mahadi Swaleh hakuhusika katika mauwaji ya Mpeketoni mwaka wa 2014.
Akitoa ushahidi wake katika mahakama kuu ya Mombasa siku ya Jumatano, Mwangi aliambia mahakama kuwa wakati wa shambulizi la Mpeketoni, alikuwa pamoja na mshukiwa Mahadi nyumbani kwake Malindi, thibitisho tosha kuwa hakuwa Lamu na hakutekeleza mauwaji hayo.
Mwangi alisisitiza kuwa madai hayo ni ya kusingiziwa na kumharibia jina Mahad.
Siku ya Jumatatu, Mahadi Swaleh alikanusha kuhusika na mauwaji hayo na kuitaja hatua hiyo kama njama ya kumchafulia jina ikizingatiwa yeye ni mfanyibiashara maarufu katika Kaunti ya Lamu.
Diana Salim, mshukiwa wa pili aliambia mahakama kuwa akiwa na wenzake walivamiwa na wanamgambo hao katika eneo la Mambosa na kulazimishwa kusoma suratul Fathia.
Diana aliongeza kuwa wenzake wawili walipigwa risasi baada ya kutambulika kuwa si Waislamu.
Alisisitiza kuwa gari zao mbili aina ya matatu zilichukuliwa na wanamgambo hao baada ya kuwavamia.
Mahadi Swaleh na Diana Salim wanakabiliwa na kesi ya ugaidi na mauwaji ya watu 60 kwenye shambulizi liliotokea Mpeketoni mwaka wa 2014.