Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Idara ya polisi mjini Nakuru sasa inatoa wito kwa kitengo cha mahakama nchini  kuwasaidia katika kutokomeza upishi na unywaji wa pombe haramu katika jimbo la Nakuru.

Idara hiyo inataka washukiwa wanaofikishwa mahakamani kwa kujihusisha na upishi, uuzaji na ulanguzi wa dawa za kulevya, wapatiwe kifungo kirefu ama faini za kiwango cha juu.

Kamishna wa jimbo la Nakuru Joshua Nkanatha amesema kuwa, inasikitisha kuona kwamba walioacha kuuza pombe hizo sasa wamezirejelea.

Nkanatha alisema hayo baada ya kuongoza zoezi la kuharibu pombe haramu katika eneo la Mwariki viungani mwa mji wa Nakuru Jumatatu, ambapo zaidi ya lita 5,000 za chang’aa zilinaswa.

“Tunapokea ripoti kwamba mshukiwa mwenye handaki hili ni mmoja wa wanaokamatwa na kufikishwa mahakamani mara kwa mara, lakini anaachiliwa baada ya kutoa faini mahakamani,” alisema Nkanatha.

Kamanda wa polisi jimbo la Nakuru Francis Kiraithe ametaka uwepo wa ushirikiano kati ya machifu na maafisa wa usalama ili kukomesha upishi na unywaji wa pombe haramu.

Chupa zenye nakala ya Kenya Wine Agency zilipatikana wakati wa zoezi hilo, ikiaminika zilikuwa zikitumika katika kupakia pombe haramu.