Mahakama ya Mombasa inatajariwa kutoa uamuzi iwapo wana wa marehemu Ibrahim Akasha na wenzao watasafirishwa hadi Marekani kufunguliwa mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Is there a story unfolding in your community? Let Hivisasa know

Baktash Akasha Abdalla, Gulam Hussein, Ibrahim Akasha Abdalla na Vijaygiri Anandgiri Goswami wanahusishwa na ulanguzi wa kilo 98 za heroini.

Hii ni baada ya mawakili wao wakiongozwa na Prof George Wajackoyah kuiambia mahakama kuwa hatua ya kuwasafirisha wateja wake nchini Marekani ni kinyume cha katiba.

“Jambo hili ni ukiukaji wa katiba ikizingatiwa tuko na mahakama zetu nchini ambazo zina uwezo wa kusikiza kesi za ulanguzi wa dawa za kulevya,” alisema Wajackoyah.

Aidha, aliongeza kuwa wateja wake walikamatwa humu nchini wala sio Marekani, hivyo hawawezi kushtakiwa nchini Marekani kulingana na katiba.

“Wateja wangu hawakutiwa mbaroni nchini Marekani. Walikamatwa humu nchini, hivyo wanafaa kushtakiwa katika mahakama za humu nchini,” alisema Wajackoyah.

Ombi hilo lilipingwa na naibu mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Alexendra Muteti, aliyesema kuwa katiba ya nchini pamoja na mikataba ya kisheria kati ya Kenya na Marekani inaruhusu washukiwa hao kufunguliwa mashtaka nchini marekani.

“Katiba iko wazi inaruhusu washukiwa kusafirishwa hadi Marekani kufunguliwa mashtaka katika nchi hiyo,” alisema Muteti.

Aidha, ameongeza kuwa mikataba ya kisheria kati ya Kenya na Marekani inaruhusu washukiwa hao kufunguliwa mashtaka nchini Marekani,” alisema Muteti.

Serikali ya Marekani inawahitaji washukiwa hao ili kuwafungulia mashtaka ya ulanguzi wa dawa za kulevya.

Uamuzi huo utatolewa Novemba 9, mwaka huu.