Mahakama Kuu itatoa uamuzi kuhusu mradi wa serikali ya Kaunti ya Mombasa wa kujenga nyumba za kisasa mwezi Disemba, mwaka huu.
Mapema mwezi wa Aprili, Gavana wa Mombasa Hassan Joho alitangaza kuwa ananuia kujenga nyumba 30,000 za kisasa, zitakazogharimu shilingi bilioni 200.
Mitaa itakayojengwa upya ni Khadija, Miritin Greenfields, Shimo la Green fields, Changamwe, Tudor, Buxton, Mzizima, Likoni na Nyerere.
Siku ya Jumatatu, wakili wa wapangaji wa maeneo hayo, Willis Oluga, aliiambia mahakama kuwa serikali ya kaunti ilikosa kuwahusisha wkaazi hao kwenye mipango ya mradi huo.
“Hakuna mazungumzo yaliyofanywa kati ya wateja wangu na serikali ya kaunti kuhusu mradi huo,” alisema Oluga.
Kwa upande wake, wakili wa serikali ya Kaunti ya Mombasa Walter Amoko alisisitiza kuwa mazungumzo yalifanyika baina ya wateja wake na wananchi.
Mahakama kuu itatoa uamuzi wake Disemba 19 mwaka huu.
Kesi hii iliwasilishwa mahakamani baada ya baadhi ya wakaazi kudai kuwa hawakuhusishwa katika mikakati ya mradi huo.
Hapo awali, mahakama kuu ilikuwa imesimamisha ujenzi wa nyumba hizo za kisasa hadi kesi iliyowasilishwa kusikizwa.