Mahakama kuu jijini Mombasa itatoa uamuzi kuhusu rufaa ya kupinga dhamana ya Haniya Saggar juma lijalo.
Saggar, ambaye ni mjane wa Sheikh Aboud Rogo na wasichana wengine watatu wanakabiliwa na madai ya kukosa kutoa ripoti kuhusu uvamizi wa kituo cha polisi cha Central.
Haya yanajiri baada ya afisi ya mkurugenzi mkuu wa mashtaka ya umma kukata rufaa kupinga dhamana ya shillingi milioni moja aliyopewa Saggar.
Naibu mkuu wa mashtaka ya umma tawi la Mombasa Alexendra Muteti, alisema Mahakama ya Shanzu ili kiuka katiba kwa kutoa dhamana hiyo ikizingatiwa uchunguzi bado unaendelea.
“Uchunguzi bado unaendelea na kuachiliwa huru kwa mshukiwa huyu kunahatarisha uhuru wa mashahidi,” alisema Muteti.
Aidha, ameongeza kuwa huenda mshukiwa huyo akatoroka vikao vya mahakama iwapo ataachiliwa huru,” alisema Muteti.
Hatua hiyo ilipingwa na wakili wa Saggar, Yusuf Aboubakar, aliyesema katiba inaruhusu mshukiwa kupewa dhamana.
“Katiba inaruhusu mshukiwa yoyote kuachiliwa kwa dhamana, na hakuna sababu ya mteja wangu kunyimwa dhamana,” alisema Aboubakar.
Aitha, alisema kuwa watoto wa Rogo wanakosa malezi bora kwa sababu mamao amezuiliwa rumande, kinyume cha katiba.
“Mteja wangu ana watoto saba ambao wanahitaji ulezi bora kutoka kwa mama yao. Watoto hao hawana raha kwani wanahuzunika kumwona mama yao rumande,” alisema Aboubakar.
Uamuzi huo utatolewa tarehe Oktoba 18, katika Mahakama kuu ya Mombasa.