Mahakama ya Kisii imetoa agizo la kuzuia serikali ya kaunti hiyo kutekeleza sheria ya fedha ya mwaka wa 2014, hadi kesi iliyowasilishwa mahakani na wafanya biashara kuhusu kodi wanayotozwa iskizwe na kuamuliwa.
Kupitia kwa kampuni ya mawakili ya Sagwe and Company, wafanya bishiara kumi na wawili wa mji wa Kisii wanateta kwamba serikali ya kaunti hiyo inatoza ushuru wa juu, na hivyo kwenda kinyume cha katiba.
Aidha, wanafanya biashara hao wanadai kuwa kodi hiyo wanayotozwa itafanya wengine wao kufunga biashara kutokana na hasara, ikizingatiwa kwamba katiba ya Kenya hairuhusu mtu yeyote kutozwa ushuru ambao ni wa juu kuliko uwezo wake.
Jaji wa mahakama kuu ya Kisii Chrispine Nagila ametoa agizo la kuzuia serikali ya kaunti chini ya uongozi wa gavana James Ongwae, naibu wake na mawaziri kuendelea kutekeleza utozaji wa kodi hizo mpya hadi kesi hiyo isikizwe na kuamuliwa.
Haijatambulika ni lini kesi hiyo itaskizwa na kudhaminiwa, huku wafanyabiashara wakiwa wamenufaika pakubwa na uamuzi huo, baada ya wengi wao kulalamikia utozwaji huo.