Share news tips with us here at Hivisasa

Wakazi kutoka mtaa wa Dunga Unuse katika eneo bunge la Jomvu wamepata nafuu baada ya mahakama makuu ya Mombasa kutoa amri siku ya Jumanne kuwa ubomozi wa makao katika eneo hilo ukome na wakazi wasifurushwe kutoka hadi kesi iliyowasilishwa kortini kutafutiwa utatuzi.

Kesi hiyo ambayo iliwasilishwa na zaidi ya familia mia mitatu ambazo ziliweza kuaathiriwa kutokana na ubomozi wa makao yao mwisho wa mwezi wa Septemba, kupitia kwenye ombi la dharura, imewapa nafuu wakazi hao ambao walikuwa wamepewa ilani ya kuhama eneo hilo ili kutoa nafasi ya mwekezaji wa binafsi kuendeleza eneo hilo.

Kulingana na hakimu aliyesilkiliza kesi hiyo Nelson Njagi, kesi hiyo ni ya dharura, hivyo basi ni muhimu ubomoaji zaidi usitishwe pamoja na watu ambao wanaishi katika eneo hilo la Dunga Unuse waachwe bila kufukuzwa mahali hapo hadi kesi hiyo itakapokamilika na kupata mwafaka kupitia korti.

Baadhi ya wakazi ambao waliongea na mwandishi habari huyu walionyesha furaha yao kufutia mahakama kutoa uamuzi huo, na kusema kuwa sasa wanaweza kuona haki yao ikishughulikiwa na mahakama hiyo.

“Nina uhakikika kuwa kesi yetu itapata utatuzi unaofaa na tunashukuru hakimu kwa kutoa mwelekeo kama huu, sasa tunaweza kupumua baada ya kuwa na wasiwasi mkubwa kuwa mnyakuzi huyo wa eneo letu angerudi kutufurusha,” alisema Charles Ogolla, mwathiriwa ambaye aliongoza wenzake kwenye kesi hiyo.