Mwenyekiti wa vuguvugu la MRC Omar Mwamnuadzi akiwa mahakamani hapo awali.[Picha/ nation.co.ke]
Mahakama ya Mombasa imeagiza kesi dhidi ya vuguvugu la MRC kuendelea licha ya kutokuwepo kwa mwenyekiti wao Omar Mwamnuadzi.Mwamnuadzi na wenzake zaidi ya 20 wanakabiliwa na mashtaka ya kuandaa mkutano kinyume cha sheria na kuwa wanachama wa kundi hilo la MRC.Hakimu Francis Kyambia aliagiza kesi hiyo kuendelea licha ya Mwamnuadzi kususia vikao hivyo.Akitoa uamuzi huo siku ya Jumanne, Hakimu Kyambia alisema sheria inaruhusu kesi kuendelea licha ya mshukiwa mmoja kukosa kuhudhuria kikao cha mahakama.“Sheria inaruhusu kesi hii kuendelea hata bila ya Mwamnuadzi kufika mahakamani,” alisema Kyambia.Uamuzi huu unajiri baada ya wakili wa vuguvugu hilo Yusuf Aboubakar kupinga kuendelea kwa kesi hiyo.Aboubakar alitaaka kesi hiyo kusitishwa ikizingatiwa kuwa Mwamnuadzi, ambaye ndiye mshukiwa mkuu katika kesi hiyo hajulikani aliko.Hata hivyo, mwendesha mashtaka Jamii Yamina aliitaka kesi hiyo kuendelea licha ya Mwamnuadzi kukosekana mahakamani.Mwamnuadzi amesusia vikao vya kesi hiyo kwa takribani miezi sita sasa, huku maafisa wa usalama wakikosa kumtia mbaroni licha ya agizo la kumkamata kutolewa.Kesi hiyo itasikizwa tarehe Februari 6, 2018.