Share news tips with us here at Hivisasa

Mahakama Kuu ya Mombasa imetoa agizo la kufunguliwa kwa akaunti za benki za mashirika mawili ya kutetea haki za kibinadamu mjini Mombasa.

Akitoa uamuzi huo siku ya Alhamisi, Jaji Anyara Emukule alisema kuwa kufungwa kwa akaunti za shirika la Muhuri na Haki Afrika ni kinyume na katiba.

Aidha, aliongeza kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi alikiuka katiba kwa kuagiza kufungwa kwa akaunti hizo, kwani hana mamlaka yoyote kikatiba ikizingatiwa kuwa waziri wa usalama pekee ndiye yuko na uwezo wa kuagiza kufungwa kwa akaunti hizo.

Vile vile, alisisitiza kuwa Inspekta Jenerali hakutoa sababu za kutosha zinazohusisha mashirika hayo na ufadhili wa ugaidi.

Wakati huo huo, viongozi wa mashirika hayo wakiongozwa na Khelf Khalifa wa Muhuri na Francis Auma wa Haki Afrika walipongeza uamuzi wa mahakama na kusisitiza kuwa haki na usawa umepatikana.

Aidha, waliongeza kuwa watashirikiana na serikali katika kutetea haki za binadamu kwa mujibu wa katiba.

Mashirika haya ni miongoni mwa mashirika ya kijamii 85 yaliyofungwa na serikali kwa tuhuma za kufadhili makundi ya kigaidi nchini, siku chache baada ya tukio la kigaidi la Chuo Kikuu cha Garisa lililotokea Aprili 2, 2015 lililopelekea watu 148 kuaga dunia na wengine 79 kupata majeraha.